Ad Code

TANGAZA NA KANKONO MEDIA HAPA 0659671919

"NO REFORM NO ELECTION AINIHUSU MIMI NITASHIRIKI UCHAGUZI "-MBUNGE WA CHADEMA JIMBO LA NKASI KASKAZINI

 



"NO REFORM NO ELECTION AINIHUSU, MIMI NITASHIRIKI UCHAGUZI "-MBUNGE WA CHADEMA JIMBO LA NKASI KASKAZINI


kankonmediablogspot.com Machi.25.2025 - NKASI - RUKWA



Nkasi Kaskazini, Tanzania – Mbunge wa Chadema wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenan, ameweka wazi msimamo wake kuwa atashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akipinga waziwazi kaulimbiu ya chama chake ya "No Reform, No Election," ambayo inasisitizwa na Mwenyekiti wa chama, Tundu Lissu.



Akihutubia wananchi wa jimbo lake, Khenan alisema kaulimbiu hiyo haina mashiko kwa sababu imeletwa kwa shinikizo la mwenyekiti, lakini haiafungi wanachama wote wa Chadema. Alieleza kuwa wengi ndani ya chama, wakiwemo baadhi ya viongozi waandamizi, hawaungi mkono wazo la kususia uchaguzi kwa sababu linaenda kinyume na sheria na linawanyima wananchi haki yao ya msingi ya kushiriki uchaguzi.


"4R za Rais Samia ndizo zilizotufanya leo tuwe na uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara bila bugudha na wasiwasi. Serikali imetengeneza mazingira mazuri ya kidemokrasia, hivyo hakuna sababu ya kususia uchaguzi. Tunasema tunataka demokrasia, halafu tunakimbia uchaguzi, hiyo haieleweki," alisema Khenan huku akishangiliwa na wafuasi wake.


Mbunge huyo alisisitiza kuwa kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Chadema kuhusu kuzuia uchaguzi hadi yapatikane mabadiliko ya kweli si tu kwamba haziwezi kufanikiwa, bali pia ni kinyume cha sheria na zinawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi.


"Hatutatumia siasa za vitisho na kususia kama silaha ya mapambano ya kisiasa. Haki ya kushiriki uchaguzi ni yetu sote, na hatuwezi kuizuia kwa sababu ya maamuzi ya mtu mmoja au kundi dogo la viongozi," aliongeza Khenan.


Msimamo wake unakuja wakati ambapo ndani ya Chadema kumekuwa na mgawanyiko kuhusu mkakati wa uchaguzi, huku wengi wakionyesha dalili za kutotii agizo la "No Reform, No Election." Wakati Mwenyekiti Lissu anasisitiza kususia uchaguzi endapo hakutakuwa na mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, baadhi ya wanachama wanaona kuwa hatua hiyo ni ya kujinyima nafasi ya kushindana na kuwakilisha wananchi.


Kwa hali ilivyo, kauli za Khenan zinaweza kuchochea mjadala mkubwa ndani ya Chadema kuhusu ushiriki wake kwenye uchaguzi ujao, huku ikiendelea kuonekana wazi kuwa si wote ndani ya chama wanakubaliana na msimamo wa mwenyekiti wao.



#KankonoMediaNewsUPDATES

Post a Comment

0 Comments